

Lugha Nyingine
UN yasema Watoto milioni 3.4 nchini Ethiopia hawaendi shuleni kwa sababu ya athari za vita na majanga ya mabadiliko ya tabianchi
ADDIS ABABA, - Zaidi ya watoto milioni 3.4 kote Ethiopia hawana fursa ya kwenda shule, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UNOCHA) imeeleza Jumatatu jioni.
Kwenye ripoti yake ya Hali ya Ethiopia, UNOCHA imesema zaidi ya watoto milioni 3.4, wakiwemo wasichana milioni 1.7, hawapati fursa ya kwenda shule kutokana na athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi nzima hiyo ya Afrika Mashariki.
UNOCHA imesema katika Jimbo la Tigray pekee, Kaskazini mwa Ethiopia, zaidi ya watoto milioni 2.3, wakiwemo wasichana milioni 1.8, hawako shuleni kutokana na kufungwa kwa shule 2,270 katika jimbo hilo.
Jimbo la Tigray limepata hasara kubwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili kati ya wanajeshi wanaoungwa mkono na serikali kuu ya Ethiopia na wanajeshi watiifu kwa Kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF). Vita hivyo vimesababisha makumi ya maelfu kuuawa, na kuwafanya mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa dharura wa ubinadamu .
Serikali ya Ethiopia na TPLF, Novemba 2, 2022, zilitia saini makubaliano ya kusitisha uhasama ili kumaliza vita hivyo.
Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa uratibu wa sekta mbalimbali unafanyika ili kusaidia kurejesha shughuli za masomo Kaskazini mwa Ethiopia, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundo na mifumo ya shule.
Hata hivyo, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema limepokea kiwango cha chini cha fedha zinazohitajika kusaidia shughuli za elimu ya dharura kote Ethiopia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma