

Lugha Nyingine
Sweden, Finland na Norway zaapa kuimarisha ushirikiano wa ulinzi (2)
STOCKHOLM, - Viongozi wa Sweden, Finland na Norway wameapa kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi siku ya Jumatano katika kukabiliana na changamoto za pamoja za usalama.
Rais wa Finland Sauli Niinisto, Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson na Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store walikutana Jumatano huko Harpsund, kwenye umbali wa kilomita 120 Kusini Magharibi mwa Stockholm, Mji Mkuu wa Sweden.
Mji wa Harpsund ni makao ya pili ya nchi ya waziri mkuu wa Sweden. Watatu hao wamejadili changamoto za usalama za pamoja na ushirikiano katika masuala ya sera za mambo ya nje, usalama na ulinzi.
Taarifa ya serikali ya Sweden iliyotolewa siku ya Jumatano imesema kuwa hali ya usalama imezorota kutokana na vita kati vya Russia na Ukraine.
"Norway, Finland na Sweden, pamoja na majirani zetu wa Nordic, wana wajibu wa pamoja wa kukabiliana na changamoto za usalama katika ukanda huu, ikiwa ni pamoja na maeneo yetu ya kaskazini," imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa Sweden na Finland ziko njiani kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi (NATO), "tunafanya kazi kwa njia iliyounganishwa zaidi ili kuimarisha usalama."
Finland na Sweden zilituma maombi ya kujiunga na NATO Mei 2022 kufuatia kuzuka kwa vita vya Russia na Ukraine. Kujiunga kwao NATO kunahitaji idhini ya nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo ya kijeshi. Uturuki na Hungary, zote wanachama wa NATO, bado hazijatoa kibali chao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma