Mavazi ya kitamaduni ya China yaonyeshwa kwa mara ya kwanza kwenye Kanivali ya Venice
VENICE, Italia - Nguo za kitamaduni za China zimeanza kwa mara ya kwanza kuonekana kwenye Kanivali ya Venice huku kukiwa na mabadilishano ya kitamaduni kati ya mji wa Suzhou wa Mashariki mwa China na mji dada wa Venice, Italia.
Jumla ya watu wa kujitolea 16 wa China na Italia, wakiwa wamevalia mavazi ya kale ya Hanfu ambayo yamekuwa yakivaliwa kitamaduni na Wachina wengi wa Kabila la Han, walishiriki katika maandamano yaliyoanzia katika eneo la Piazza San Marco katikati mwa mji huo wenye rasi.
"Hii ni mara ya kwanza kwa mavazi ya kitamaduni ya China kuonekana rasmi katika kanivali," amesema Ma Xiaohui, mkurugenzi wa upande wa China wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Ca' Foscari cha Venice.
Ma amesema, nguo hizo, zilizosafirishwa moja kwa moja kutoka Jumba la Makumbusho ya Hariri la Suzhou, zilikuwa na dalizi na mapambo ya enzi za Han, Tang, Song na Ming, zikionyesha vyema utamaduni wa Sehemu za Kusini mwa Eneo la Mto Changjiang na hariri ya Suzhou inayojulikana duniani.
“Nimeamua kushiriki kwenye shughuli hii baada ya kuiona kupitia mtandao wa Instagram” Amesema Irene De Maio kutoka Mji wa Sicily, Kusini mwa Italia. “Nilidhani ni namna ya kuuleta utamaduni wa China karibu name” ameongeza.
Onyesho hilo la mavazi ya kijadi ya China limevutia vijana wengi kutoka China na Italia.
" Shughuli hizo ni za kushangaza, haswa ile kuhusu Suzhou, mji ambao naupenda sana," mtalii wa Serbia, aliyeishi Suzhou kwa miaka minne amesema.
Mji wa Suzhou, uliopewa jina la "Venice ya Mashariki" na mvumbuzi wa Italia Marco Polo katika Karne ya 13, ulitangazwa kuwa mji dada wa Venice Mwaka 1980, na tangu wakati huo shughuli nyingi za mabadilishano ya kihistoria na kitamaduni zimeendelezwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma