

Lugha Nyingine
Watu zaidi ya 30,000 wamefariki hadi sasa kwenye matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea Uturuki na Syria huku uokoaji wa ajabu ukileta matumaini (3)
ANKARA/DAMASCUS - Idadi ya watu waliofariki kutokana na matetemeko mawili ya ardhi yaliyokumba Uturuki na Syria Tarehe 6 Februari imeongezeka na kufikia watu 29,605 na 1,414 hadi jana Jumapili jioni.
Wakati huo huo, Idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka hadi zaidi ya 80,000 nchini Uturuki na 2,349 nchini Syria, kwa mujibu wa takwimu rasmi.
Ujenzi mbovu
Uturuki imetoa amri ya kuwakamata washukiwa 134 waliohusika katika ujenzi mbovu wa majengo yaliyoporomoka kutokana na tetemeko la ardhi, Waziri wa Sheria wa Uturuki Bekir Bozdag amesema Jumapili.
“Watatu miongoni mwa washukiwa hao wameshamatwa,” Bozdag amewaambia waandishi wa habari.
Matetemeko hayo makubwa ya ardhi yamebomoa zaidi ya majengo 20,000 katika majimbo 10 yaliyoathiriwa na tetemeko hilo.
Yavuz Karakus na Sevilay Karakus, wakandarasi wa majengo mengi yaliyoharibiwa kwenye tetemeko la ardhi katika Jimbo la Adiyaman, Kusini mwa Uturuki, walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Istanbul walipokuwa wakijaribu kutorokea Georgia, shirika la utangazaji la NTV limeripoti Jumapili.
Watu wawili zaidi wamekamatwa kwa kukata nguzo za jengo lililoporomoka katika Jimbo la Gaziantep, Shirika la Habari la Uturuki, Anadolu limeripoti.
Uokoaji unaendelea
Maelfu ya waokoaji wanaendelea kutafuta dalili zozote za uwepo wa watu walio hai katika majengo mbalimbali ya ghorofa yaliyoporomoka katika siku ya saba ya maafa hayo. Matumaini ya kupata watu wakiwa hai yanafifia, lakini timu bado zinafanya uokoaji wa ajabu.
Waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca alichapisha mtandaoni video ya mtoto wa kike aliyeokolewa saa 150 baada ya tetemeko la ardhi kutokea. "Ameokolewa muda mfupi uliopita na kikosi cha waokoaji. Kuna matumaini daima!" ameandika kwenye mtandao wa Twitter.
Misada ua usaidizi wa kimataifa
Shehena ya kwanza ya misaada ya dharura, ikiwa ni pamoja na mahema na blanketi, iliyotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi imewasili Uturuki siku ya Jumamosi.
Syria pia inapokea vifaa kutoka kwa Chama cha Msalaba Mwekundu cha China na jumuiya ya makazi ya Wachina nchini humo.
Siku ya Jumapili, Algeria na Libya pia zilituma ndege zilizojaa vitu vya msaada kwa maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma