

Lugha Nyingine
Watu wengine wawili walionusurika kwenye tetemeko la ardhi waokolewa kufuatia juhudi za pamoja za waokoaji wa China na Uturuki
ANTAKYA, Uturuki - Vikosi vya uokoaji vya China na Uturuki kwa pamoja siku ya Alhamisi vimewaokoa watu wengine wawili walionusurika kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka katika eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi lililotokea Antakya, mji ulio katika Jimbo la Hatay, Kusini mwa Uturuki.
Wanawake hao wawili waliwekwa sehemu salama zaidi ya saa 72 muhimu za uokoaji, waandishi wa Shirika la Habari la China, Xinhua wameshuhudia katika eneo la tukio.
Mapema siku hiyo, mwanamke mjamzito aliokolewa na waokoaji kutoka kwenye jengo la ghorofa nane lililoporomoka huko Antakya, amesema Zhao Yang, naibu kiongozi wa kikosi cha uokoaji cha China.
Wakati huo huo, miili ya watu wawili waliofariki ilipatikana majira ya Saa 5:50 Asubuhi kwa saa za Ankara (0850 GMT) siku ya Alhamisi baada ya waokoaji wa China kufanya juhudi.
Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter na matetemeko yake ya baadaye yalitokea katika Kusini mwa Uturuki na Kaskazini mwa Syria siku ya Jumatatu, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 14,014 huko Uturuki na 3,556 nchini Syria hadi sasa, kwa mujibu wa takwimu za hivi punde.
Waokoaji wa kimataifa wanakimbia dhidi ya wakati kutafuta dalili za uwepo wa watu walio hai katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko. Vikosi kadhaa vya utafutaji na uokoaji kutoka China vimewasili na mbwa wa uokoaji, vifaa vya uokoaji na vifaa vingine vya msaada kusaidia katika juhudi hizo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma