

Lugha Nyingine
Idadi ya waliofariki kwenye tetemeko la ardhi katika Uturuki na Syria yazidi 8,000, huku Marekani ikitakiwa kuiondolea vikwazo Syria (4)
![]() |
Watu wakitafuta waathirika walionusurika kwenye vifusi vya jengo lililobomolewa katika tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika Mji wa Demsarkho, Jimbo la Latakia, Kaskazini-Magharibi mwa Syria Februari 7, 2023. (Str/Xinhua) |
ANKARA/DAMASCUS - Idadi ya watu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu huko Uturuki na Syria imeongezeka hadi kufikia 8,364, kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na mamlaka husika na waokoaji leo Jumatano.
Idadi ya hivi punde ya waliofariki kutokana na matetemeko makubwa ya ardhi nchini Uturuki imefikia 5,894 na majeruhi wapatao 34,810, Shirika la Habari la Uturuki, Anadolu limeripoti Jumatano, likimnukuu Makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay akisema.
Nchini Syria, takriban watu 2,470 wametangazwa kufariki na 2,050 kujeruhiwa, imesema Wizara ya Afya ya Syria.
Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter limelikumba Jimbo la Kahramanmaras, Kusini mwa Uturuki siku ya Jumatatu saa 10.17 alfajiri kwa saa za huko (0117 GMT). Tetemeko hilo, lilifuatiwa na tetemeko lingine lenye ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter dakika chache baadaye katika Jimbo la Gaziantep, Kusini mwa nchi hiyo na tetemeko lingine la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richter saa Saa 7. 24 Mchana kwa saa za huko (1024 GMT) katika Jimbo la Kahramanmaras.
Wito kwa Marekani kuiondolea vikwazo Syria
Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria siku ya Jumanne ilikosoa vikwazo vya Marekani kwa kuzuia kazi ya huduma za kibinadamu na shughuli za uokoaji katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.
Katika taarifa yake, wizara hiyo imesema kuwa Wasyria, wakati huu wakikabiliana na janga la tetemeko la ardhi, wanachimba kati ya vifusi kwa mikono yao wenyewe au kwa kutumia zana duni zaidi kwani vifaa vya kuondoa vifusi hivyo vimepigwa marufuku kutokana na vikwazo vya Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran siku ya Jumanne ilitoa wito kwa nchi mbalimbali kuishinikiza Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Syria.
Misaada yazidi kumiminika
Siku mbili baada ya tetemeko hilo kubwa la ardhi, nchi nyingi zaidi zimejiunga kwenye juhudi za uokoaji na utoaji misaada zinazoendelea Syria na Uturuki.
Nchi za Kiarabu zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Jordan, Lebanon, Misri, Iran sambamba na nyinginezo duniani kote zimetangaza kutoa usaidizi na misaada ya aina mbalimbali.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma