

Lugha Nyingine
Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi imeongezeka hadi zaidi ya 4000 huko Uturuki na Syria (6)
![]() |
Watu wakitafuta manusura kwenye vifusi vya jengo lililobomolewa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika Wilaya ya Pazarcik, Jimbo la Kahramanmaras, Uturuki, Februari 6, 2023. (Picha na Mustafa Kaya/Xinhua) |
ANKARA/DAMASCUS – Zaidi ya watu 4,000 wamefariki na wengine makumi ya maelfu kujeruhiwa hadi kufikia leo Jumanne mchana baada ya matetemeko makubwa ya ardhi kukumba maeneo ya Uturuki na nchi jirani ya Syria mapema Jumatatu, wakati timu za uokoaji zikipambana na hali mbaya ya msimu wa baridi kutafuta manusura.
Mamlaka ya Kukabiliana na Majanga na Dharura ya Uturuki (AFAD) imesema, idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi Jumatatu imeongezeka na kufikia zaidi ya 2,921 hadi leo Jumanne mchana, huku timu za uokoaji zikifanya kazi kwa haraka kuokoa watu walionaswa chini ya vifusi katika hali ya hewa ya baridi na mvua.
AFAD pia imebainisha kuwa watu wasiopungua 15,834 wamejeruhiwa na zaidi ya majengo 5,606 kubomolewa baada ya kutokea kwa matetemeko makubwa ya ardhi, na kuongeza kuwa jumla ya watu 14,720 kwa sasa wanaendelea kutoa msaada katika eneo la maafa, ikiwa ni pamoja na wanajeshi.
Katika nchi jirani ya Syria, takriban watu 711 wameuawa hadi sasa na 1,431 kujeruhiwa katika majimbo ya Aleppo, Latakia, Hama, Tartus, imesema Wizara ya Afya ya Syria. Habari za vyombo vya habari pia zimewanukuu waokoaji wakisema kuwa watu 733 wameuawa na zaidi ya 2,100 kujeruhiwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi nchini Syria.
Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter limelikumba Jimbo la Kahramanmaras, Kusini mwa Uturuki saa 10.17 alfajiri kwa saa za huko (0117 GMT). Tetemeko hilo, lilifuatiwa na tetemeko lingine lenye ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter dakika chache baadaye katika Jimbo la Gaziantep, Kusini mwa nchi hiyo na tetemeko lingine la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richter saa Saa 7. 24 Mchana kwa saa za huko (1024 GMT) katika Jimbo la Kahramanmaras.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Jumatatu alitangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kwa waathrika wa matetemeko hayo ya ardhi.
"Kipindi cha maombolezo ya kitaifa cha siku saba kimetangazwa. Bendera yetu itapandishwa nusu mlingoti hadi machweo ya Jumapili, Februari 12, 2023, katika ofisi zetu zote za serikali na za wawakilishi wa nje," Erdogan aliandika kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Twitter.
Tetemeko hilo la ardhi la Jumatatu linaaminika kuwa kubwa zaidi nchini Uturuki tangu kutokea kwa tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 katika kipimo cha Richter kwenye Jimbo la Erzincan, Mashariki mwa Uturuki ambalo liliua watu 33,000 Mwaka 1939.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma