Wapalestina wapinga ziara ya Blinken huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya Waisraeli na Wapalestina
RAMALLAH/GAZA - Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan imezua hasira miongoni mwa Wapalestina wengi, ambao waliandamana Jumanne kuelezea hisia zao za kupinga kuwepo kwa mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani katika ardhi ya Palestina.
Waandamanaji katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza, walinyanyua bendera za Palestina na kutamka kaulimbiu mbalimbali za hamasa dhidi ya Marekani, zinazoituhumu nchi hiyo kuwa na upendeleo kwa Israel na ukiukaji wake wote wa haki za Wapalestina.
"Suala ni rahisi sana, Blinken amekuja hapa kushinikiza uongozi wa Palestina kutopitisha uamuzi wowote dhidi ya ushirikiano wa kiusalama na Israel," amesema Nael Salama, ambaye alishiriki kwenye maandamano hayo katika mji wa Ramallah wa Ukingo wa Magharibi ya Mto Jordan akiwa amebeba bango linalosomeka "Marekani ni mhalifu tu ilimradi inaiunga mkono Israel."
"Tumekuja hapa kuwasilisha ujumbe wetu kwa Blinken kwamba hakaribishwi katika nchi yetu” Issam Baker, mratibu wa vikosi vya kitaifa na vya Kiislamu huko Ramallah, ameliambia Shirika la Habari la Xinhua.
Amesisitiza kuwa serikali ya Marekani inatumia "undumilakuwili" katika kushughulikia suala la Palestina, na kuongeza kwamba "itasababisha tu kuendelea zaidi kwa mduara wa vurugu."
Tangu kuanza Mwaka 2023, vikosi vya Israeli vimewaua Wapalestina 35, na kuifanya Januari kuwa moja ya miezi yenye idadi kubwa zaidi ya vifo vya watu kwenye Ukingo wa Magharibi ya Mto Jordan katika miaka ya hivi karibuni. Israel inasema mashambulizi yake yalilenga kuwazuia wanamgambo wapalestina kupanga mashambulizi.
Katika kulipiza kisasi, mtu mmoja wa Palestina alitumia bunduki kufyatua risasi nje ya sinagogi katika makazi ya Waisraeli huko Jerusalem Mashariki na kusababisha Waisrael saba kupoteza maisha.
Mapema jana, Blinken alifanya mkutano na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwenye makao makuu ya Rais wa Palestina huko Ramallah baada ya mikutano yake na viongozi wa Israel siku ya Jumatatu.
Blinken amewataka Wapalestina na Waisraeli wote kutuliza mivutano huku akisisitiza ahadi ya Washington yenye "uimara wa chuma" ya kujitolea kwa usalama wa Israeli.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma