

Lugha Nyingine
Mauzo nje ya silaha ya Marekani yaongezeka kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa fedha wa 2022 (2)
![]() |
Picha iliyowekwa mtandaoni na Wizara ya Ulinzi ya Marekani Agosti 23, 2022 ikionyesha shehena ya mizigo ya silaha inayoelekea Ukraine ikiwa imepakiwa katika Kambi ya Kijeshi ya McGuire-Dix-Lakehurst, New Jersey, Marekani. (Picha kwa hisani ya ukurasa wa Twitter wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani) |
WASHINGTON - Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zimeonesha kuwa, Mauzo ya nje ya silaha ya Marekani yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa fedha wa 2022, ongezeko hilo hasa lilitokana na msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine wakati huu wa mgogoro kati ya Ukraine na Russia.
Thamani ya jumla ya mauzo ya nje ya kijeshi yaliyoidhinishwa na Wizara ya Mambo ya Nje kutoka kwa serikali hadi serikali ilikuwa dola za Kimarekani bilioni 51.9 katika mwaka wa fedha wa 2022, katika kipindi cha miezi 12 kilichoishia Septemba 30, 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 49.1 kutoka dola bilioni 34.8 za mwaka uliopita, takwimu hizo zimeonyesha.
Kile kinachojulikana kama mauzo ya moja kwa moja ya kibiashara, au mauzo ya silaha na zana za kijeshi kwa serikali za nje na wakandarasi wa ulinzi wa Marekani, pia yaliongezeka katika mwaka wa fedha wa 2022, na kuongezeka kwa asilimia 48.6 hadi dola bilioni 153.7, ikilinganishwa na dola bilioni 103.4 katika mwaka wa fedha wa 2021.
Mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2022, mashirika 14,445 yalisajiliwa katika Idara ya Udhibiti wa Biashara inayohusika na Ulinzi wa Nchi ili kufanya shughuli za biashara hiyo, ambayo inawakilisha ongezeko kidogo kutoka mwaka wa fedha wa 2021, wizara hiyo imesema katika habari zilizotolewa nayo Jumatano.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema, ongezeko hilo limetokana na utoaji endelevu wa Marekani wa usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine katikati ya mgogoro unaoendelea kati ya Ukraine na Russia, huku ikidai kuwa "uhamishaji wa silaha na biashara inayohusika na ulinzi wa nchi ni nyenzo muhimu za sera ya mambo ya nje ya Marekani."
Kwa mujibu wa habari mpya zilizotolewa na Wizara ya Ulinzi Jumatano, Marekani imetumia zaidi ya dola bilioni 27.1 za usaidizi wa ulinzi na usalama kwa Ukraine tangu mgogoro kati ya Russia na Ukraine ulipoanza Februari 24, 2022.
Kuhusiana na mahali ambapo mauzo hayo ya silaha ya Marekani yanahitajika na kuhusika zaidi, ni kwa washirika na wenzi wa Marekani barani Ulaya, huku mahitaji ya silaha za Marekani yakiongezeka hasa katika nchi za Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), na katika maeneo ya Asia Pasifiki na Mashariki ya Kati.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma