

Lugha Nyingine
Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha Nepal ateuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Nepal
KATHMANDU - Pushpa Kamal Dahal, mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha Nepal (Chenye mrengo wa Maoist), ameapa kuchukua wadhifa wa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo Jumatatu mchana.
"Rais Bidya Devi Bhandari amemuapisha kiapo cha kushika wadhifa Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal," Sagar Acharya, msemaji wa Ofisi ya Rais huko Kathmandu, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Manaibu mawaziri wakuu watatu na mawaziri wanne pia wamekula kiapo leo,” amesema.
Manaibu mawaziri wakuu watatu ni Bishnu Poudel kutoka Chama cha Kikomunisti cha Nepal (Chenye Mrengo wa Umarx Ulioungana), Narayan Kaji Shrestha kutoka CPN (Mrengo wa Maoist) na Rabi Lamichhane kutoka Chama cha Rastriya Swatantra, ambaye pia anashika nyadhifa za mambo ya fedha, miundombinu na usafiri na mambo ya ndani.
Dahal, ambaye pia anajulikana kwa jina la Prachanda, aliteuliwa kuwa waziri mkuu Jumapili jioni na rais baada ya kupata uungaji mkono wa wabunge 169 katika Baraza la Wawakilishi lenye jumla ya wabunge 275.
Waziri mkuu huyo mpya sasa anahitaji kushinda kura ya kuwa na imani naye katika baraza la mawaziri ndani ya siku 30.
Muungano huo mpya wa vyama vinavyounda serikali na kujumuisha vyama saba vya kisiasa una mawaziri wengine watatu kutoka CPN-UML na mmoja kutoka Chama cha Janamat.
Hakuna chama kati ya hivyo kilichoweza kushinda wingi wa viti katika bunge la chini katika uchaguzi mkuu wa Novemba 20.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma