

Lugha Nyingine
Waziri wa Fedha wa Uingereza atangaza kuongeza kodi, kupunguza matumizi ili kurejesha hali ya kifedha ya umma
LONDON - Waziri wa Fedha wa Uingereza Jeremy Hunt Alhamisi ametangaza hatua kadhaa za kuongeza kodi na kupunguza matumizi yenye thamani ya pauni bilioni 55 za Uingereza (kama dola za Marekani bilioni 65) katika jitihada za kuboresha hali ya kifedha ya umma na kurejesha uaminifu kwa uchumi wa nchi hiyo.
Kupunguza bajeti
"Leo tunatoa mpango wa kukabiliana na msukosuko wa gharama za maisha na kujenga upya uchumi wetu," Hunt ameliambia Bunge la Commons katika Taarifa yake ya Majira ya Vuli Mwaka 2022. "Vipaumbele vyetu ni utulivu, ukuaji wa uchumi na huduma za umma."
Kwa mujibu wa waziri huyo, ili kuongeza mapato zaidi, kiwango cha juu ambacho watu wa kipato cha juu wataanza kulipa kiwango cha juu cha asilimia 45 kitapunguzwa kutoka pauni 150,000 hadi pauni 125,140, wakati ushuru wa mapato, ushuru wa urithi na vikomo vya bima ya taifa vitasimamishwa kwa miaka miwili zaidi hadi Aprili, 2028.
Ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanaopata faida kubwa kutokana na bei ya juu ya nishati pia wanalipa viwango stahiki, ushuru wa malipo kwa makampuni ya mafuta na gesi utaongezeka kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35, na ushuru ukisalia hadi Machi 2028, na tozo mpa ya muda ya asilimia 45 itaanzishwa kwa jenereta za umeme.
Kuhusu matumizi ya fedha za umma, wizara zitatarajiwa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuunga mkono dhamira ya serikali ya nidhamu ya kifedha. Kuanzia Mwaka 2025-2026 na kuendelea, matumizi ya kila siku yataongezeka polepole zaidi kwa asilimia 1 juu ya mfumuko wa bei.
Mtazamo mbovu wa kiuchumi
"Waziri amesimamia kauli yake katika kuangazia utulivu wa kifedha na kulenga msaada kwa walio hatarini zaidi katika jamii. Lakini katika meno ya mdororo wa uchumi, kauli hii haitaongeza imani kwenye biashara," Shevaun Haviland, mkurugenzi mkuu wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Uingereza (BCC), ametoa maoni.
Siku ya Alhamisi, Ofisi ya Uangalizi wa Uwajibikaji wa Bajeti (OBR) ilisema katika mtazamo wake mpya wa kiuchumi na kifedha kwamba kupanda kwa bei kutapunguza mishahara halisi na kupunguza viwango vya maisha kwa asilimia 7 kwa jumla katika kipindi cha miaka miwili ya fedha hadi 2023-2024, na kufuta kabisa ukuaji wa miaka minane iliyopita, licha ya msaada wa serikali.
Imesema, kufinywa kwa mapato halisi, kupanda kwa viwango vya riba na kushuka kwa bei ya nyumba kutaathiri uzito wa matumizi na uwekezaji, na hivyo kuuingiza uchumi katika mdororo uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kutoka robo ya tatu ya 2022.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma