Mkutano wa COP27 wafunguliwa Misri huku ukitaka ahadi za fedha kuwa vitendo, ajenda ya ufadhili wa uharibifu wa tabianchi yaingizwa rasmi
SHARM EL-SHEIKH, - Mkutano wa 27 wa Nchi Washiriki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) umefunguliwa Jumapili katika mji wa pwani wa Sharm El-Sheikh nchini Misri kwa matumaini ya kugeuza ahadi za kimataifa za ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi kuwa hatua na kuingiza kwa mara ya kwanza ufadhili wa hasara na uharibifu wa tabia nchi katika ajenda.
Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Mwenyekiti wa COP27, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliohusu ufunguzi wa mkutano huo kwamba anafurahi kuona washirika wa COP27 wakikubali kuanzisha ufadhili wa hasara na uharibifu wa tabia nchi kuwa ajenda, na kuongeza kuwa Dunia inahitaji "mduara wa ubora ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi."
Akitoa hotuba yake kwenye hafla za ufunguzi, Shoukry amesisitiza haja ya kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano huo utakaoendelea kwa wiki mbili, ambapo zaidi ya viongozi 120 wa Dunia watatafuta ufumbuzi unaowezekana wa changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
"Mabadiliko ya tabianchi yanatishia maisha ya binadamu, na mtindo wa maendeleo katika sekta ya viwanda ambao siyo endelevu lazima ubadilishwe kwa sababu hii itasababisha matokeo mabaya," Shoukry ameonya.
"Tumeshuhudia katika mwaka huu matukio ya uchungu nchini Pakistan, Bara la Afrika na sehemu mbalimbali za Ulaya na Amerika. Matukio haya yote na uharibifu na athari zinawakilisha somo la kujifunza na kutisha duniani kote ... kwa tahadhari zaidi, na kuchukua hatua haraka kuchukua hatua zote muhimu kulingana na makubaliano na ahadi zetu," amesema.
Mwenyekiti huyo wa COP27 pia amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wahusika wasio wa serikali, ikiwa ni pamoja na sekta ya kibinafsi, benki, taasisi za fedha za kimataifa, mashirika ya kiraia, vyama vya vijana na vyama vya kienyeji, kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa ahadi na makubaliano.
"Juhudi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika miongo kadhaa iliyopita ziligawanywa kwa njia ya kushangaza, ambayo imepunguza kasi ya mazungumzo," Shoukry amesema, huku akiongeza kuwa ahadi ya kukusanya dola za Kimarekani bilioni 100 kwa mwaka bado haijatekelezwa.
Wakati huo huo, Alok Sharma, Mwenyekiti wa COP26 iliyofanyika Glasgow, Scotland, amehimiza haja ya umoja ili kufanya lengo la halijoto katika digrii 1.5-Celsius kufikiwa, akiangazia jukumu muhimu ambalo ufadhili na uwezekezaji vitakalochukua katika mkutano huo.
"Tunajua kwamba tumefikia hatua ambapo fedha hufanya au kuvunja maendeleo ya programu iliyo mbele yetu," amebainisha.
"Mkutano huu lazima uwe juu ya hatua madhubuti na ninatumai viongozi wa Dunia watakapoungana nasi leo, wataelezea kile ambacho nchi zao ziliafiki katika mwaka uliopita na jinsi watakavyosonga mbele," mwanasiasa huyo wa Uingereza amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma