Makala: Fundi makanika wa magari wa kike wa Tanzania aushinda ulimwengu wa wanaume
![]() |
Jane Goodluck Isowe akifanya kazi kwenye karakana yake ya ukarabati wa magari Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam, Tanzania, Agosti 22, 2022. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua) |
DAR ES SALAAM - "Hakuna kitu kama kazi zinazotawaliwa na wanaume katika msamiati wangu. Ufundi magari kwa muda mrefu umeonekana kama ulimwengu wa wanaume," anasema Jane Goodluck Isowe, mwanamke anayemsimamia karakana ya ukarabati wa magari iliyoko Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Isowe, mwenye umri wa miaka 49, amekuwa akiendesha karakana yake ya kukarabati magari tangu Mwaka 1994, akiwavutia wateja wa kike na wa kiume wanaotembelea mahali pake kwa ajili ya kukarabati magari yao.
"Jamii zetu zinadhani kuwa kuna kazi, ikiwa ni pamoja na ufundi wa magari, kwa ajili ya wanaume pekee. Kwangu mimi hii ni ndoto ya mchana. Wanawake wanaweza kufanya kazi yoyote inayofikiriwa kuwa ya wanaume ikiwa wanaamua kufanya hivyo," Isowe ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.
"Timu yangu, wengi wao wakiwa wanafunzi wa mafunzo, na mimi hukarabati gari moja hadi mawili kwa siku. Tunakarabati breki, gia, injini na vifaa vya kutofautisha kasi," anasema fundi huyo mwanamke wakati akifanya kazi ya kukarabati gari. "Wateja wangu wengi wananiamini na wanapongeza kazi yangu kila wakati."
Isowe anasema mpaka sasa amewafunza wanawake watatu waliohitimu ufundi stadi na sasa wameajiriwa katika karakana tofauti za kukarabati magari.
Mbali na wanawake hao watatu, Isowe anasema pia amewafundisha ufundi magari vijana wa kiume zaidi ya 50 ambao wamepata ajira kwenye karakana mbalimbali.
Anasema safari yake ya kuwa fundi magari mahiri ilianza Mwaka 1989 alipohama kutoka Marangu mkoani Kilimanjaro hadi jiji kuu la biashara Dar es Salaam.
"Lakini kabla sijahamia Dar es Salaam nilianza kupenda magari nikiwa mdogo sana. Niliunda midori ya magari kwa plastiki," anasema.
Anasema, alipofika Dar es Salaam, alianza maisha yake kwa kuishi na shemeji yake aliyekuwa akifundisha Chuo Kikuu cha Ardhi. "Shemeji yangu alikuwa na gari na nilikuwa nikimuuliza kazi za sehemu mbalimbali za gari lake."
Shemeji yake na familia yake baadaye walihamia nchini Canada na Isowe aliamua kujiunga na chuo cha kidini cha kozi ya ukatibu muhtasi hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 alipoanza kuingia kwenye karakana ya kukarabati magari.
Alimuuliza mmiliki wa karakana hiyo aliyemtaja kwa jina la Eugene Mushi kama anaweza kujiunga na karakana yake na kupata mafunzo ya ufundi makanika wa magari.
"Mmiliki alishangaa na kuniuliza imekuwaje mwanamke kama mimi kutaka kujifunza ufundi makanika," anasema Isowe, akithibitisha tena kuwa umakanika ulikuwa chaguo lisilo la kawaida kwa wanawake kujitosa.
"Baada ya kuanza kwa shida kama fundi wa magari, watu sasa wanafurahi kuniona nafanya kazi ya ufundi," anasema Isowe na kuongeza kuwa anatazamia kupata eneo kubwa ili aweze kupanua karakana yake.
Anasema pia anatarajia kupata zana za kisasa za kuboresha biashara yake lakini ni ghali sana.
Isowe ametaja mafanikio ambayo amepata kutokana na biashara yake, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba bora, kununua gari lake binafsi, na kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu zaidi ya 50.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma