China yaimarisha mifumo ya kuunga mkono watu wenye ulemavu katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano
BEIJING - Mamilioni ya watu wanaoishi na ulemavu wameshuhudia maisha yao yakiboreka huku China ikipiga hatua kubwa katika ufikiaji, ujumuishaji na uungaji mkono wakati wa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025) ambapo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Beijing Jumanne, maofisa wakuu kutoka Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu la China (CDPF) wamefahamisha mafanikio makubwa katika uungaji mkono kwa watu wenye ulemavu wakati wa kipindi hicho na kuelezea malengo mapya kwa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030)
"Kiwango cha watoto na vijana wenye ulemavu kupata elimu ya lazima nchini China kimefikia asilimia 97, huku wanafunzi zaidi ya 30,000 wenye ulemavu wakiingia vyuo vikuu kila mwaka," amesema Cheng Kai, mwenyekiti wa CDPF, kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.
Mpango ujao wa miaka mitano umepangwa kuweka kipaumbele katika maendeleo bora ya hali ya juu katika mambo ya watu wenye ulemavu, kwa mujibu wa mkutano huo na waandishi wa habari.
Cheng amesema, mfumo wa elimu wa China kwa watu wenye ulemavu umeboreshwa zaidi ambapo hivi sasa, wanafunzi 75,800 wenye ulemavu wanasoma katika shule za sekondari za ufundi stadi nchi nzima, huku 59,800 wakisoma shule za sekondari za kawaida.
Li Dongmei, naibu mwenyekiti wa shirikisho hilo, amesema kuwa kampeni maalum ilizinduliwa kwa ajili ya kuziwezesha kampasi za shule vifaa saidizi, ikinufaisha wanafunzi karibu 100,000 wenye ulemavu. Aidha ameeleza kuwa, vitabu vya kiada vilivyosanifiwa vimetayarishwa kwa ajili ya shule za elimu maalum, vilevile vitabu vya lugha ya ishara kwa masomo tisa.
"Kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika bima ya msingi ya matibabu nchini China kimeendelea kuwa zaidi ya asilimia 95. Wakati huo huo, asilimia zaidi ya 90 ya watu wenye ulemavu nchini China wanashiriki kwenye bima ya msingi ya pensheni kwa wakazi wa mijini na vijijini," amesema Cheng.
Amesema, hadi kufikia Juni 2025, ruzuku kwa watu wenye ulemavu wenye matatizo ya kifedha na ruzuku za matunzo kwa watu wenye ulemavu mkubwa zimenufaisha watu milioni 11.88 na milioni 16.4, mtawalia.
"Jumla ya watu milioni 10.5 wenye ulemavu wako katika mfumo wa posho ya kujikimu nchini," Cheng ameongeza.
Cheng amesema, huduma za umma pia zimeimarishwa ili kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu ambapo kampeni ya kitaifa ya ukarabati nyumba bila vizuizi vya walemavu ilinufaisha familia milioni 1.28 zenye watu wenye ulemavu mkubwa katika kipindi hicho, ikivuka lengo la awali la milioni 1.1.
Zhou Changkui, mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa CDPF, amesema wakati China ikiweka dira ya Mpango wa 15 wa Miaka Mitano, maendeleo bora ya hali ya juu katika mambo ya watu wenye ulemavu unaendelea kuwa jambo la msingi, huku kukiwa na msisitizo katika mifumo imara zaidi ya uungaji mkono na suluhu zinazotokana na uvumbuzi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma