

Lugha Nyingine
Barabara zafungwa katika sehemu ya mji mkuu wa Uganda kabla ya maandamano yaliyopangwa
Wanajeshi na polisi wakikamata waandamanaji kwenye maandamano ya kupinga ufisadi huko Kampala, mji mkuu wa Uganda, Julai 23, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA - Polisi wa Uganda Jumanne walifunga barabara kadhaa muhimu zinazoelekea katika jengo la bunge la nchi hiyo ambako waandamanaji walikuwa wamepanga siku hiyo kuandamana kuelezea kutofurahishwa kwao na kile wanachokiita ufisadi uliokithiri serikalini.
Magari ya umma hayaruhusiwi kwenye barabara hizo, ambazo zinaweza kufikiwa tu na watembea kwa miguu ambao lazima wapitie ukaguzi mkali wa usalama.
Wanajeshi na polisi walikuwa wakionekana kushika doria kwa miguu barabarani huku magari ya kijeshi yakiwa kwenye njia muhimu za makutano mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda.
Luke Owoyesigire, naibu msemaji wa polisi wa Mji wa Kampala, amesema katika mahojiano ya simu na Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba hali katika mji huo ni ya kawaida, ingawa askari wa usalama wametumwa.
Wanaharakati wamekuwa wakihamasisha watu kupitia mitandao ya kijamii kuandamana hadi bungeni siku hiyo Jumanne. Polisi wameapa kuzuia maandamano hayo, wakibainisha kwamba wahalifu wanaweza kuyatumia kusababisha fujo.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema mwishoni mwa wiki kuwa wahusika kutoka nchi za nje walikuwa wanafanya kazi na upinzani kusababisha vurugu nchini humo kupitia migomo, maandamano haramu na shughuli zisizofuata utaratibu.
Bunge la Uganda siku ya Jumatatu lilisema liko tayari kupokea ombi litakalowasilishwa na wawakilishi wa waandamanaji, ingawa halitahusika na kile kitakachotokea kwa watu nje ya bunge wakati wakiandamana.
Polisi wakiwa wamesimama kupiga doria kwenye Barabara ya Bunge huko Kampala, mji mkuu wa Uganda, Julai 23, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma