Madaktari wa China waleta huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Ethiopia
Zhang Jing (mbele), daktari mkuu kutoka Timu ya 9 ya Madaktari wa Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) nchini Ethiopia, akiangalia rekodi za matibabu ya mgonjwa kwenye Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi huko Addis Ababa, Ethiopia, Juni 23, 3023. (Xinhua/Wang Ping)
ADDIS ABABA - Gezahegn Tilahun alikuwa akisumbuliwa na kile alichokiita kuwa ni "ugonjwa wa ajabu" kwa miaka zaidi ya miwili kabla ya kulazwa katika Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
"Kwa mara ya kwanza nilianza kuhisi maumivu nilipokuwa zamu kwenye mapigano makali Kaskazini mwa Ethiopia," amesema Tilahun, alipokuwa akikumbuka mateso aliyopitia kutokana na maumivu ya tumbo yaliyokuwa yakizidi kuongezeka kwa muda kabla ya kupata wakati wa kwenda kituo cha afya kilichoko karibu.
"Nilipewa rufaa ya kwenda hospitali nne, na hakuna hata moja iliyogundua sababu halisi ya ugonjwa wangu. Madaktari katika kila hospitali waliniambia kuwa ugonjwa wangu ulikuwa vigumu kutibika na kunipa rufaa kwenda hospitali ya ngazi ya juu," amesema.
Kutokana na huo, mwili wa Tilahun ulipoteza uzito wa kilo 21, na baada ya muda, ngozi na macho yake yaligeuka kuwa ya njano. Akiwa katika kipindi hicho kigumu, madaktari wa Timu ya Madaktari ya Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) nchini Ethiopia walimtembelea Tilahun na kutathmini hali yake huku akiwa amelazwa katika Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi.
Daktari Bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo Tena Mamo amesema Tilahun aligunduliwa kuwa na uvimbe kwenye kongosho, ambao hospitali hiyo haikuwahi kufanya upasuaji wa aina hiyo hapo awali.
"Tulikuwa tunapanga kumpa rufaa mgonjwa huyu kwenda Hospitali ya Black Lion (hospitali kubwa zaidi ya rufaa nchini Ethiopia), ambapo orodha ya wanaosubiri huduma ni ndefu sana. Kama isingekuwa uwepo wa Daktari Wang, nina uhakika tusingeweza kufanya upasuaji kwa mgonjwa huyu," Mamo amesema.
Wang Xiaojun ni kiongozi wa Timu ya 9 ya Madaktari wa China wa PLA nchini Ethiopia, yenye makao yake katika Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi.
Hatimaye, timu ya madaktari wa upasuaji wa Ethiopia na China walifanikiwa kufanya upasuaji tata ambao ulichukua muda wa saa nane na hatimaye kuokoa maisha ya Tilahun.
"Ni upasuaji wa kwanza tuliofanya wa uvimbe wa kongosho katika hospitali yetu. Tumemfanyia mgonjwa upasuaji bila shida yoyote na hakuna matatizo," daktari huyo kijana wa Ethiopia amesema.
Bamlak Tessema, mwamuzi maarufu wa kimataifa wa mchezo wa mpira wa miguu aliye na uzoefu wa kushiriki Kombe la Dunia la FIFA Mwaka 2022 na Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, ni mmoja wa Waethiopia wengi ambao wanatumia matibabu ya kijadi ya acupuncture kwa msaada wa madaktari wa China.
"Tunawashukuru Wachina (madaktari) kwa uhamishaji wa ujuzi na uzoefu huu, na kisha madaktari wetu wataendelea na hilo." amesema.
Wang Xiaojun (kushoto), kiongozi wa Timu ya 9 ya Madaktari wa Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) nchini Ethiopia, na daktari wa upasuaji Tena Mamo (M) wakizungumza na mgonjwa kwenye Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi huko Addis Ababa, Ethiopia, Juni 23, 3023. (Xinhua/Wang Ping)
Wang Xiaojun (kushoto), kiongozi wa Timu ya 9 ya Madaktari wa Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) nchini Ethiopia, akiangalia afya ya mgonjwa katika Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi huko Addis Ababa, Ethiopia, Juni 23, 3023. (Xinhua) /Wang Ping)
Liu Yueqiu, mtaalamu wa tiba ya asili ya acupuncture kutoka Timu ya 9 ya Madaktari wa Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) nchini Ethiopia, akimtibu mgonjwa kwa njia ya tiba hiyo kwenye Hospitali Maalumu ya Vikosi vya Jeshi huko Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 23 Juni 3023. (Xinhua/Wang Ping)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma