Rais wa Iran kuzuru Saudi Arabia
Rais wa Irani Ebrahim Raisi akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Tehran, Iran, Agosti 29, 2022. (Tovuti ya Ikulu ya Irani/ Xinhua)
TEHRAN - Rais wa Iran Ebrahim Raisi amekubali mwaliko kutoka kwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudi Arabia wa kufanya ziara katika Mji Mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber amethibitisha Jumatatu.
Shirika la Habari la Mehr la Iran limeripoti kuwa Mokhber aliyasema hayo alipojibu swali kuhusu mwaliko wa Mfalme wa Saudia kwa Raisi wa kuzuru Riyadh
Mwaliko huo umekuja baada ya mazungumzo ya suluhu kati ya pande hizo mbili yaliyoongozwa na China hapa Beijing mapema Mwezi Machi, ambapo Saudi Arabia na Iran zilikubali kurejesha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na kufungua tena ubalozi na ujumbe wa kidiplomasia katika pande hizo ndani ya miezi miwili.
Machi 19, Mohammad Jamshidi, naibu mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Irani kwa maswala ya kisiasa, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba mfalme wa Saudi Arabia amemwandikia barua ya mwaliko rais wa Iran kutembelea Riyadh.
Akizungumzia uhusiano wa Iran na Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu katika eneo hilo, Mokhber alisema kuboreshwa kwa uhusiano na nchi za eneo hilo imekuwa miongoni mwa mikakati mikubwa inayofuatiliwa na serikali ya Raisi tangu rais huyo aingie madarakani.
Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mwanzoni mwa Mwaka 2016 ikiwa ni kuchukua hatua baada ya mashambulizi dhidi ya ujumbe wa kidiplomasia wa Saudia nchini Iran baada ya ufalme huo kumhukumu kifo kasisi wa Kishia.?
Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud akitoa hotuba yake ya kufunga kwenye mkutano wa Kundi la 20 (G20) Riyadh, Saudi Arabia, Novemba 22, 2020. (G20 Saudi Arabia/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma