Wataalamu watoa wito kwa Afrika kuziba pengo la kiteknolojia ili kurahisisha mageuzi ya nishati
Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Uchumi wa Afrika (UNECA) imetoa taarifa ikisema wataalamu wametoa wito kwa nchi za Afrika kuziba pengo lililopo la kiteknolojia katika bara zima ili kurahisisha mageuzi ya nishati.
Wito huo umetolewa kwenye mazungumzo ya ngazi ya juu ya sera katika Kongamano la 5 la Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu la Afrika kuhusu Teknolojia za Nishati Zinazoibuka ambayo yalikutanisha wataalamu wa Afrika na Umoja wa Mataifa Februari 26 na 27 huko Addis Ababa, Ethiopia.
Wataalamu hao wametoa wito wa kufanya marekebisho ya kina barani Afrika katika masuala ya nishati ili kuondoa mzunguko mbaya wa teknolojia zilizopitwa na wakati, na kuwezesha ufanisi zaidi na mahitaji ya umeme na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Nishati Mbadala na Ufanisi wa Nishati cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Bw. Francis Sempore, wazo la nishati ya kijani inayotokana na haidrojeni katika eneo la Afrika Magharibi linaweza kuonekana ni dhahania kwa sasa, kama ilivyo kwa uamuzi wa viongozi wa ECOWAS wa kupitisha sera ya kikanda ya nishati mbadala Mwaka 2013. Hata hivyo, amesema bado ni jambo lisilofikirika kwa nchi kutokuwa na nishati ya jua katika mchanganyiko wake wa nishati.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma