

Lugha Nyingine
Uchaguzi wa rais nchini Cyprus waingia kwenye duru ya mwisho
Mwanamke akipiga kura kwenye kituo cha kupigia kura huko Nicosia, Cyprus, Februari 5, 2023. Wapiga kura nchini Cyprus walipiga kura siku ya Jumapili kumchagua rais mpya atakayechukua nafasi ya Rais anayemaliza muda wake Nicos Anastasiades. (Picha na George Christophorou/Xinhua)
NICOSIA - Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Cyprus Nicos Christodoulides ametangazwa kuongoza katika uchaguzi wa rais wa Cyprus siku ya Jumapili, na atachuana na Andreas Mavroyiannis, ambaye ameibuka mshindi wa pili, katika duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika Februari 12.
Christodoulides, ambaye aligombea akiwa mgombea huru bila uwakilishi wowote wa chama cha siasa, amepata asilimia 32.04 ya kura zote zilizopigwa, na Mavroyiannis, ambaye pia aligombea akiwa mgombea huru asiyewakilisha chama chochote cha siasa na kuungwa mkono na chama cha mrengo wa kushoto cha AKEL, amepata asilimia 29.61 ya kura zote, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Costas Constantinou ametangaza baada ya kuhesabu kura zote siku ya Jumapili.
Wagombea kumi na wanne wameshiriki katika uchaguzi huo, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepata kura nyingi za kuweza kutangazwa kuwa mshindi.
Averof Neophytou, kiongozi wa chama tawala cha DISY, ameshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 26.11 ya kura zote na hivyo kuachwa nje ya kinyang'anyiro cha urais, na hivyo kumaliza kipindi cha miaka kumi cha utawala wa chama hicho katika kisiwa hicho cha Mashariki mwa Mediterania.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba wagombea hao wawili waliobaki wataanza kuwashawishi wapiga kura wa Chama cha DISY ili kupata uungwaji mkono wao kabla ya uchaguzi wa mwisho.
Afisa mmoja wa DISY amesema chama hicho kitakutana Jumatatu ili kuamua msimamo wake rasmi kuhusiana na uchaguzi huo wa mwisho.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi amesema kati ya wapiga kura 561,273 waliojiandikisha ni watu 404,403 sawa na asilimia 72.05 waliopiga kura.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma