

Lugha Nyingine
Mamia ya watu wafanya maandamano katika Mji wa New York kupinga vita
Mtoto akiwa amebeba bango lenye maandishi ya kupinga vita kwenye maandamano katika eneo la Times Square, New York, Marekani, Januari 14, 2023. (Picha na Ziyu Julian Zhu/Xinhua)
NEW YORK - Mamia ya waandamanaji kutoka Jiji la New York, Marekani na maeneo ya karibu wamefanya maandamano na mikutano ya hadhara kupinga ushiriki wa Marekani kwenye vita katika maeneo na nchi mbalimbali duniani kote kwenye eneo la Times Square siku ya Jumamosi.
Washiriki walizungumza dhidi ya upanuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) na kutoa wito wa kupatikana amani nchini Ukraine, wakikosoa matumizi makubwa ya Marekani katika mgogoro wa Ukraine na tangazo la Ikulu ya White House kuipatia Kiev makombora mengine ya Patriot yanayofyatuka kutoka ardhini hadi angani.
"Tuko hapa leo kwa sababu tunapinga upanuzi usio na kikomo wa NATO, ambao siyo tu hauna ulazima lakini ni wa kutojali na wa kichochezi," amesema Brian Becker, mkurugenzi wa taifa wa Muungano wa ANSWER, shirika kubwa la kupinga vita nchini Marekani.
Mtoto akiwa amebeba bango lenye maandishi ya kupinga vita kwenye maandamano katika eneo la Times Square, New York, Marekani, Januari 14, 2023. (Picha na Ziyu Julian Zhu/Xinhua)
Badala ya kuzidisha vita na kutuma silaha zaidi nchini Ukraine, Marekani inapaswa kurejea kwenye meza ya mazungumzo na kutambua kwamba Russia ina madai na masuala halali ya kiusalama, Becker ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kando ya mkutano huo.
"Sisi pia tuko hapa leo kwa sababu Marekani inatumia ziada ya dola za Marekani bilioni 65 kufadhili vita nchini Ukraine wakati kuna watu mamilioni wasio na makazi hapa Marekani, wakati shule zetu hazina fedha na watu wengi wanafilisika kwa sababu wanashindwa kulipa bili za madaktari,” amesema Becker, ambaye ameitaka nchi yake kutumia pesa hizo kusaidia Wamarekani wenye mahitaji badala ya kufadhili vita na masuala ya kijeshi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma