

Lugha Nyingine
Shirika la Hali ya Hewa la Duniani lasema miaka 8 iliyopita ilikuwa yenye joto zaidi kuwahi kutokea
Picha hii iliyopigwa Tarehe 11 Novemba 2022 ikionyesha kipimajoto kinachoonyesha halijoto ya muda halisi ikiwa nyuzi joto 21 huko Rome, Italia. (Xinhua/Jin Mamengni)
GENEVA - Kuongezeka kwa viwango vya hewa chafu na mkusanyiko wa joto kumesababisha miaka minane iliyopita kuwa yenye halijoto ya kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limesema Alhamisi.
Kwa mujibu wa data za halijoto zilizokusanywa na WMO, Mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa nane mfululizo ambapo halijoto ya kila mwaka duniani ilifikia angalau nyuzijoto moja juu ya viwango vya kabla ya viwanda.
Mkataba wa kihistoria wa Tabianchi wa Paris wa Mwaka 2015 uliahidi kuendelea kuweka ongezeko la joto duniani "chini ya" nyuzi joto mbili juu ya viwango vya kabla ya kuwa na maendeleo makubwa ya viwanda, na kujitahidi kupunguza kiwango cha halijoto kwa nyuzi joto 1.5.
Wakati huo huo, Jopo la Kiserikali la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) limesisitiza kuwa halijoto inayoongezeka duniani inapaswa kupunguzwa hadi nyuzi joto 1.5 au chini ya hapo.
Watu wakitumia muda kwenye ufukwe wa bahari huko Faliro, kitongoji cha Kusini mwa Athens, Ugiriki, Januari 6, 2023. Ugiriki imekuwa na halijoto isiyo ya kawaida msimu huu wa baridi, na kuwafanya watu waelekee kwenye ufukwe huo badala ya vituo vya kuteleza kwenye theluji. (Xinhua/Marios Lolos)
Hata hivyo, data za hivi punde za WMO zimeonyesha kuwa wastani wa joto duniani Mwaka 2022 ulikuwa karibu nyuzi joto 1.15 juu ya viwango vya kabla ya viwanda, wakati wastani wa halijoto ya miaka kumi katika kipindi cha Mwaka 2013 hadi 2022 ulikuwa nyuzi joto 1.14 juu ya kiwango cha kabla ya viwanda.
Hii inaonyesha kuwa kuongezeka kwa halijoto kwa muda mrefu kunaendelea, na uwezekano wa kukiuka kwa muda lengo la nyuzi joto 1.5 unaongezeka, imesema WMO.
Mawimbi ya joto kali, ukame na mafuriko makubwa yaliathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni ya fedha Mwaka 2022, kwa mujibu wa ripoti ya muda ya WMO ya Tabianchi Duniani Mwaka 2022.
Picha hii iliyopigwa Agosti 15, 2022 ikionyesha mwonekano wa hifadhi ya Cijara huko Extremadura, Hispania. (Xinhua/Meng Dingbo)
"Kuna haja ya kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na matukio hayo makali na kuhakikisha kuwa tunafikia lengo la Umoja wa Mataifa la Tahadhari ya Mapema kwa Wote katika miaka mitano ijayo," Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma