Kuweka vizuizi vya kusafiri kwa abiria wanaowasili kutoka China "haina uhalali wa kisayansi": ACI Tawi la Ulaya
Kituo cha kupima UVIKO-19 kilichofungwa kikionekana katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow huko London, Uingereza, Machi 18, 2022. (Xinhua/Li Ying)
PARIS – Kufanya upimaji UVIKO-19 kwa abiria kabla ya kuondoka au wanapowasili kutoka China "hakujathibitishwa kisayansi wala hakuna msingi wa hatari," Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege, Tawi la Ulaya (ACI-Ulaya) limesema hivi karibuni.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Desemba 31, 2022, baraza hilo limeonyesha "masikitiko yake kuhusu hatua za mataifa kadhaa ndani ya EU (Umoja wa Ulaya) na kimataifa kwa kuweka kwa upande mmoja masharti ya usafiri yanayohusiana na afya."
"Hatua hizi za upande mmoja zinapingana na uzoefu na ushahidi wote uliopatikana katika miaka mitatu iliyopita," imesema taarifa hiyo, na kuongeza kuwa "vizuizi hivi vya kusafiri havifanyi kazi."
Mhudumu wa afya akimdunga dozi ya nyongeza ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 mkazi mwenye umri wa miaka 86 katika Eneo la Chaoyang, Beijing, China, Julai 13, 2022. (Xinhua/Ju Huanzong)
ACI-Ulaya imeeleza kuwa, kutofaulu kwa vizuizi vya kimataifa vya usafiri katika kuzuia kuenea kwa UVIKO-19 na aina zake nyingi za virusi zinazofuatiliwa (VOCs) kumetambuliwa bila shaka na Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Baraza hilo limesema, kadiri nchi zinavyohitaji kuwa macho kuhusu hali na udhibiti wa virusi, ndivyo lengo linavyopaswa kuwa katika kuongeza mpangilio wa jeni za virusi ili kutambua aina mpya zinazowezekana za COVID-19 na ufuatiliaji unaohusiana.
"Mtazamo kama huo, kama ulivyohimizwa na Kamishna wa Afya wa EU (Stella) Kyriakides katika barua iliyotumwa mapema wiki hii kwa nchi wanachama, hauhitaji wasafiri kupimwa, lakini inaweza kupatikana kwa njia kama vile kupima maji machafu kutoka kwenye viwanja vya ndege, " Taarifa ya ACI-Ulaya kwa vyombo vya habari imesema.
"Kwa mara nyingine tena tunarudi katika safu ya vizuizi vya usafiri visivyo na msingi na visivyoratibiwa, ambavyo havina msingi wa ukweli wa kisayansi," ametoa maoni Olivier Jankovec, mkurugenzi mkuu wa ACI-Ulaya.
Abiria akitembea katika eneo la abiria wa kimataifa wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow mjini London, Uingereza, Machi 18, 2022. (Xinhua/Li Ying)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma