

Lugha Nyingine
WHO yasema inatumai Tangazo la Dharura ya Afya ya Kimataifa ya UVIKO-19 litamalizika mwaka ujao
Watu wakitembea kulipita bango lenye tangazo linaloelekeza kuhusu barakoa katika duka la New York, Marekani, Tarehe 7 Desemba 2022. (Picha na Michael Nagle/Xinhua)
GENEVA - Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema Jumatano anatumai kuwa UVIKO-19 hautakuwa tena dharura ya afya duniani wakati wowote mwaka ujao.
Akihutubia mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema Kamati ya Dharura ya WHO kuhusu UVIKO-19 itajadili mwezi ujao vigezo vya kutangaza kumalizika kwa dharura ya UVIKO-19.
"Tunatumai kuwa wakati fulani mwaka ujao, tutaweza kusema kwamba UVIKO-19 siyo dharura ya afya ya kimataifa," amesema.
Hata hivyo, ameongeza kwamba virusi vya SARS-CoV-2, ambavyo ndivyo vimesababisha janga la UVIKO-19, havitaondoka.
"Viko hapa kuishi nasi, na nchi zote zitahitaji kujifunza kudhibiti ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine ya kupumua ikiwa ni pamoja na mafua na RSV (Respiratory Syncytial Virus), ambayo kwa sasa yanazunguka sana katika nchi nyingi," amesema.
Wahudumu wa afya wakimsaidia mgonjwa Bibi Li mwenye umri wa miaka 101 aliye na UVIKO-19 wakati akiondoka katika Hospitali Kuu ya Pili ya Guangzhou ya Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Novemba 26, 2022. (Hospitali Kuu ya Pili ya Mkoa wa Guangdong/Kutumwa Xinhua)
Mkuu huyo wa WHO amesema somo muhimu zaidi kutokana na janga hili ni kwamba nchi zote zinahitaji kuimarisha mifumo yao ya afya ya umma ili kujiandaa, kuzuia, kugundua na kukabiliana haraka na milipuko, magonjwa ya milipuko na yale ya kudumu.
Somo jingine muhimu ni hitaji la ushirikiano wenye nguvu zaidi katika kufanya kazi kwa pamoja, badala ya ushindani na mkanganyiko ambavyo vilitawala kwenye mwitikio wa kimataifa kwa UVIKO-19.
Wakati huo huo, Maria Van Kerkhove, kiongozi wa kiufundi wa Mpango wa Dharura wa Afya wa WHO, ameonya mawimbi ya maambukizi na maambukizi tena yataendelea kote duniani, kwani idadi ya vifo vipya vya kila wiki vinavyoripotiwa na nchi bado ni kati ya 8,000 hadi 10,000.
Mwanamke akiweka ua kwenye Ukuta wa Taifa wa Kumbukumbu za UVIKO-19 huko London, Uingereza, Machi 27, 2022. (Xinhua/Li Ying)
Mike Ryan, mkurugenzi mtendaji wa Mpango wa Dharura wa Afya wa WHO, ameonya kwamba Dunia bado haijui jinsi virusi vya SARS-CoV-2 vitakavyobadilika katika siku zijazo, na kutokuwa na uhakika kama kutaongeza hatari.
Kabla ya Mkurugenzi Mtendaji wa WHO kumaliza tangazo la dharura ya UVIKO-19, usawa unahitaji kuwekwa kati ya virusi -- ikijumuisha athari zake na kutotabirika -- na "ikiwa tumeshughulikia udhaifu na masuala ya uhimilivu katika mifumo yetu ya afya," Ryan amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma