

Lugha Nyingine
Balozi wa China nchini Marekani akanusha madai ya "mtego wa madeni" barani Afrika
Balozi wa China nchini Marekani Qin Gang (Kulia) akizungumza wakati wa majadiliano ya ana kwa ana, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa majadiliano yaliyoandaliwa na Semafor, mjini Washington, D.C., Marekani, Desemba 12, 2022.(Xinhua/Liu Jie)
WASHINGTON - Balozi wa China nchini Marekani siku ya Jumanne alikanusha madai kwamba China inatengeneza "mtego wa madeni" barani Afrika, akisema kuwa bara hilo linapaswa kuwa mahali pa ushirikiano wa kimataifa, badala ya kuwa uwanja ambapo nchi kubwa zinashindana kwa manufaa ya siasa za kijiografia.
Balozi Qin Gang aliyasema hayo katika siku ya kuamkia mkutano wa kilele unaaoandaliwa na Serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden ukiwakutanisha viongozi wa mataifa 49 ya Afrika na Umoja wa Afrika mjini Washington.
"Uwekezaji na usaidizi wa kifedha wa China kwa Afrika siyo mtego, bali ni manufaa ," Qin amesema kwenye majadiliano ya ana kwa ana, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa majadiliano yaliyoandaliwa na Semafor kujiandaa kwa Mkutano wa Kile wa Marekani na Afrika unaotarajiwa kufanyika Jumanne hadi Alhamisi. Semafor ni chombo kipya cha habari cha Marekani kilichoanzishwa mapema mwaka huu.
"Katika miongo kadhaa iliyopita, China imetoa mikopo kusaidia Afrika katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kazi za ujenzi ziko kila mahali barani Afrika," Qin amesema. "Unaweza kuona hospitali, barabara kuu, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo. Ni wazi, hakuna mtego kama huo. Siyo njama. Ni wazi, ni ya dhati."
Akitoa mfano wa utafiti uliochapishwa mwezi Julai na Debt Justice, shirika la kutoa misaada la Uingereza, Qin amesema kiasi cha deni ambacho nchi za Afrika zinadaiwa na wakopeshaji binafsi wa Magharibi ni mara tatu ya kiasi zinachodaiwa na China, na viwango vya riba kwenye mikopo ya kibinafsi ni mara mbili ya ile ya mikopo ya China.
Qin amesema, matokeo hayo, ni uthibitisho kwamba "China siyo mkopeshaji mkubwa wa deni la Afrika," na kwamba "deni ambalo China inadai ni sehemu ndogo tu."
Akitaja Mpango wa Kusimamisha Huduma ya Madeni ulioanzishwa na Kundi la 20 (G20), Qin amesema China ni mshiriki hai katika mpango huo, baada ya kusimamisha malipo mengi zaidi ya huduma ya deni kati ya wanachama wa G20.
"Tunatoa wito kwa wadai wengine wote, taasisi za kimataifa za mtandao na wakopeshaji wa kibinafsi kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza mzigo wa madeni wa nchi za Afrika kwa kufuata kanuni ya kugawana mizigo sawa na kuchukua hatua za pamoja," amesema.
Kuhusu Mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Marekani na Afrika, balozi huyo amesema angependa kuona Washington "inakuja na hatua halisi zaidi na zinazoweza kutekelezeka" zinazolenga kuhimiza maendeleo na ustawi wa Bara la Afrika.
Qin ametoa wito kwa Marekani kushirikiana na China ili nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa duniani na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ziungane katika kuhimiza amani, usalama na ustawi barani Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma