Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China asema China inatumai Uingereza itahimiza ushirikiano wa pande mbili
BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian Jumatano amesema kuwa China inatumai Uingereza itaweka mazingira ya kibiashara yenye haki kwa makampuni ya China na mazingira mazuri ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Zhao ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari alipojibu swali kuhusu mpango wa uwekezaji wa serikali ya Uingereza katika mradi wa nishati ya nyuklia wa Sizewell C na makubaliano na Kampuni ya China ya General Nuclear Power kujiondoa kwenye mradi huo.
Akinukuu kauli ya msemaji wa Ubalozi wa China nchini Uingereza, Zhao amesema China inaheshimu uamuzi wa kampuni ya China.
Katika miaka ya hivi karibuni, China, Uingereza na Ufaransa zimefanya ushirikiano katika miradi kadhaa ya miundombinu ya nyuklia nchini Uingereza, ambayo kwa ujumla inaendelea mbele, Zhao amesema.
"Tunatumai kuwa Uingereza itaweka mazingira ya biashara yenye usawa, haki na yasiyobagua makampuni ya China na mazingira mazuri ya ushirikiano kati ya China na Uingereza," Zhao amesema.
Akijibu kauli za Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak kwamba China inatoa "changamoto ya kimfumo" kwa maadili na maslahi ya Uingereza, Zhao amesema China inafuata sera huru ya mambo ya nje ya amani, na ni mshirika wa maendeleo na fursa kwa nchi nyingine, siyo tishio au changamoto.
"Tunakuza uhusiano wetu na nchi nyingine kwa msingi wa kuheshimiana na ushirikiano wa kunufaishana, na kutetea kwa dhati uhuru, usalama na masilahi yetu ya maendeleo," Zhao amesema.
Upande wa Uingereza unahitaji kutupilia mbali mawazo ya Vita Baridi, kuacha kueneza kile kinachoitwa "tishio la China," na kuiangalia China na uhusiano wake na China katika mrengo sahihi na wenye mantiki, Zhao ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma