

Lugha Nyingine
WHO yabadilisha jina la ugonjwa wa Monkeypox kuwa "mpox" ili kuepuka unyanyapaa
GENEVA - Ili kuepusha dhana potofu za kibaguzi na unyanyapaa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limependekeza Jumatatu kwamba virusi vya Monkeypox vipewe jina jipya la "mpox."
Majina yote mawili -- mpox na monkeypox -- yatatumika kwa wakati mmoja kwa mwaka mmoja huku hilo la Monkeypox likiondolewa, WHO imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari. Mabadiliko hayo yamekuja kutokana na baadhi ya watu na nchi kueleza kutoridhishwa na jina hilo katika mikutano kadhaa na kuitaka WHO kupendekeza njia ya kubadilisha jina hilo.
Kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kitatumika kupunguza wasiwasi wa wataalam kuhusu mkanganyiko unaosababishwa na mabadiliko ya jina katikati ya mlipuko wa kimataifa wa virusi hivyo. Pia kinatoa muda wa kukamilisha mchakato wa kuhuisha Uainishaji wa Kimataifa wa Magonjwa (ICD) na kuhuisha machapisho ya WHO.
Mwezi Julai mwaka huu, WHO ilitangaza rasmi mlipuko wa mpox katika nchi nyingi nje ya maeneo ya maambukizi barani Afrika kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa (PHEIC), ikiwa ni ngazi ya juu ya tahadhari ambayo mamlaka ya afya duniani inaweza kutoa.
Ni jukumu la WHO kutoa majina kwa magonjwa mapya na yaliyopo kupitia mchakato wa mashauriano, unaojumuisha nchi wanachama wa WHO. Mashauriano hayo kuhusu mpox yamehusisha wawakilishi kutoka kwa mamlaka ya serikali ya nchi 45 tofauti, imesema.
Kwa mujibu wa WHO, hadi kufikia Jumamosi, nchi wanachama 110 zilikuwa zimeripoti maambukizi 81,107 yaliyothibitishwa na maabara na visa 1,526 vinavyoshukiwa, pamoja na vifo 55. Visa vingi vya mpox vilivyoripotiwa katika wiki nne zilizopita vilitoka Bara Amerika (asilimia 92.3) na Ulaya (asilimia 5.8). Idadi ya visa vipya vilivyoripotiwa kila wiki duniani ilipungua kwa asilimia 46.1 katika wiki ya Novemba 21-27.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma