Algeria yasisitiza kuunga mkono juhudi za Cuba za kuondoa vikwazo
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune (Kulia) akikutana na Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel mjini Algiers, Algeria, Novemba 17, 2022. Abdelmadjid Tebboune Alhamisi amesisitiza "mshikamano wa kudumu" wa Algeria na Cuba katika mapambano ya Cuba ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa kwa zaidi ya miongo sita. (Ikulu ya Algeria/Kutumwa kwa Xinhua)
ALGIERS - Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amesisitiza "mshikamano wa kudumu" wa Algeria na Cuba katika mapambano ya Cuba ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa kwa zaidi ya miongo sita.
Tebboune ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel anayezuru mjini Algiers, ambapo wamejadili ushirikiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.
"Nchi hizi mbili zina uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu na mshikamano ambao una alama ya maadili ya uhuru, amani na haki," Rais wa Algeria amesema.
Amesisitiza "mshikamano wa kudumu wa watu wa Algeria na Cuba," ambao wanajitahidi kuondoa vikwazo vya kiuchumi, kifedha na kibiashara vilivyowekwa kwa nchi yao kwa zaidi ya miaka 60, "kwa kufuata imani yetu katika kanuni na madhumuni ya Umoja wa Mataifa na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutaka kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Cuba."
Tebboune amesema kuwa Algeria imeamua "kupunguza mzigo kwa uchumi wa Cuba kupitia kufuta viwango vyote vya riba ya madeni ya Cuba kwa Algeria na kuahirisha malipo yake."
Algeria pia "itatoa mtambo wa nishati ya jua na kurejesha usambazaji wa hidrokaboni kwa Cuba ili kuiwezesha kuwasha tena mitambo iliyozimwa," ameongeza.
Kwa upande wake, Rais Diaz-Canel amesema "Algeria na Cuba ni mfano wa kuigwa katika uhusiano wao wa kirafiki, mshikamano na kusaidiana tangu Mwaka 1963, wakati Cuba ilipotuma timu ya wahudumu wa afya kutoa msaada kwa watu ndugu wa Algeria."
Amesema kuwa ziara yake hiyo inayoambatana na maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ina umuhimu mkubwa.
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune (Kulia, Mbele) akimkaribisha Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel (kati, mbele) mjini Algiers, Algeria, Novemba 17, 2022. (Ikulu ya Algeria/Kutumwa kwa Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma