Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito wa kufikia makubaliano kuhusu hatua za Tabianchi kwenye COP27
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Utekelezaji wa Hatua za Kubabiliana na Tabianchi ya Sharm El-Sheikh (SCIS) kwenye Mkutano wa 27 wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa (COP27) huko Sharm El-Sheikh, Misri, Novemba 7, 2022. (Xinhua/Sui Xiankai)
SHARM EL-SHEIKH, Misri - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Alhamisi ametoa wito kwa nchi kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi badala ya "kunyoosha vidole" katika mkutano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Mkutano wa 27 wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP27), ambao umepangwa kufungwa leo Ijumaa katika mji wa pwani wa Sharm El-Sheikh nchini Misri.
Guterres amesema kuwa COP27 itafikia kikomo leo Ijumaa, lakini ni wazi kuna "kuvunjika" kwa kuaminiana kati ya Kaskazini na Kusini.
Hakuna wakati wa kunyoosheana vidole, amesema, huku akiongeza "mchezo wa lawama ni kichocheo cha uharibifu wa uhakika."
Mwanamke akipiga picha mbele ya bango linaloonyesha Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP27) huko Sharm El-Sheikh, Misri, Novemba 6, 2022. (Xinhua/Sui Xiankai)
Kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Guterres amezitaka pande husika kuchukua hatua katika maeneo matatu muhimu – mwitikio juu ya hasara na uharibifu, kupunguza pengo la utoaji wa hewa chafu, na kutoa mitaji inayohitajika.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kutoa dola za kimarekani bilioni 100 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea na kuweka dira ya kuaminika ya ufadhili maradufu wa uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Ameweka bayana kuwa nchi zilizoendelea "lazima" kutoa msaada ambao nchi zinazoendelea zinahitaji kuendeleza nishati mbadala na kuimarisha uwezo wao wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
"Nishati mbadala ni njia za kutoka kwenye barabara kuu ya kuelekea kuzimu ya tabianchi," amesema, huku akirejea kauli zake za awali kuhusu kile kinachoitwa "barabara kuu ya kuelekea kuzimu ya tabianchi" aliyoitoa kwenye mkutano wa viongozi wa COP27.
Guterres ametoa wito wa kufikia muafaka haraka katika COP27, akionya kwamba "saa ya tabianchi inayoyoma na uaminifu unaendelea kupotea."
Kwenye mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Mwenyekiti wa COP27 Sameh Shoukry amesisitiza kwamba bado kuna masuala kadhaa yanayokosa maendeleo katika hatua ya mwisho ya COP27.
Pande husika "zinakwepa kuchukua maamuzi magumu ya kisiasa," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma