

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China atoa wito wa ushirikiano katika Asia Mashariki ili kuhimiza amani na ustawi
Waziri Mkuu wa China Li Keqiang akihudhuria kwenye Mkutano wa 17 wa Wakuu wa nchi za Asia Mashariki huko Phnom Penh, Cambodia, Novemba 13, 2022. (Xinhua/Yue Yuewei)
PHNOM PENH - Waziri Mkuu wa China Li Keqiang Jumapili katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Asia Mashariki (EAS) ametoa wito wa kubadilishana fursa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kufikia amani ya muda mrefu, utulivu na ustawi katika Asia Mashariki.
Waziri Mkuu Li aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa 17 wa EAS ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Cambodia Samdech Techo Hun Sen na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Umoja wa Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN), Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol, Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern, Makamu wa Rais wa India Jagdeep Dhankhar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov na viongozi wengine.
Waziri Mkuu Li amesema hali ya kimataifa na kikanda ni yenye utatanishi, huku kukiwa na hatari za nishati, chakula na mambo ya fedha na changamoto zinapamba moto. Wakati huo huo, kanda hiyo imedumisha amani na utulivu kwa ujumla, huku ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda ukiendelea kusonga mbele na umeundwa mfumo thabiti wa viwanda na ugavi.
“Wakati wito wa amani na maendeleo miongoni mwa watu katika kanda unazidi kuimarika, nchi za kanda hiyo zinahitaji kuheshimiana, kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana, na kukabiliana na hatari na changamoto pamoja,” amesema.
Kwa maana hiyo, Waziri Mkuu wa China ametoa mapendekezo matatu.
Kwanza, nchi zinahitaji kudumisha mazungumzo ya kimkakati na kufanya maingiliano yenye kujenga. Likiwa ni jukwaa la kimkakati linaloongozwa na viongozi, EAS inapaswa kutumika kama jukwaa la mazungumzo ili kuhimiza ushirikiano na mashauriano kati ya nchi za kikanda ili kuongeza maelewano na kuaminiana, na kudhibiti tofauti ipasavyo, amesema.
Nchi za kikanda zinapaswa kuepuka kutengana, na bado zipunguze kuelekea kwenye makabiliano, amesema. “China iko tayari kushirikiana na pande nyingine zote ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kupanua na kuimarisha ushirikiano wa kivitendo na kuimarisha msingi wa amani na utulivu wa kudumu katika Asia Mashariki.
Pili, nchi zinahitaji kufuata ushirikiano wa kunufaishana na kukabiliana na hatari na changamoto kwa pamoja.
Waziri Mkuu Li amesema kuwa pande zote zinapaswa kufuata mwelekeo sahihi wa utandawazi wa uchumi na kuendelea kufuata biashara na uwekezaji huria na urahisi, kufanya kazi kwa utekelezaji mzuri wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda (RCEP), kuweka minyororo ya viwanda na ugavi salama, thabiti na rahisi, na kusukuma mbele mchakato wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
“China inaamini kuwa ni muhimu kulinda nishati na usalama wa chakula, kufanya juhudi za pamoja ili kukabiliana na changamoto za hali ya hewa na ikolojia, na kuendeleza maendeleo endelevu katika eneo hilo” ameeleza.
Tatu, nchi zinahitaji kushikilia umuhimu wa Umoja wa Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN) na kujenga muundo wa kikanda ulio jumuishi.
Waziri Mkuu Li amesema kuwa muundo wa ushirikiano wa kikanda unaoongozwa na ASEAN unashughulikia maslahi ya pande zote na unaendana na hali halisi ya kikanda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma