AU yatoa wito wa uingiliaji kati wa kivitendo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa viwanda barani Afrika
ADDIS ABABA - Albert Muchanga, Kamishna wa Umoja wa Afrika wa Maendeleo ya Kiuchumi, Biashara, Utalii, Viwanda na Madini ametoa wito wa kuingilia kati kwa vitendo ili kuongeza kasi ya mabadiliko katika ukuaji wa viwanda wa Afrika ulio shirikishi na endelevu.
Kamishna huyo wa AU ameyasema hayo kwenye mkutano wa pamoja wa mawaziri wa Afrika wanaosimamia viwanda na mseto wa uchumi ambao umefanyika katika mji mkuu wa Niger, Niamey siku ya Jumatatu, taarifa ya AU imeeleza.
"Tuupe uhai na kasi kubwa ukuaji wa viwanda barani Afrika ulio shirikishi na uendelevu kupitia hatua za kivitendo ambazo zitaleta matokeo yanayopimika na yanayoonekana ya ubunifu, ushindani, pato, uongezaji thamani, ajira, miongoni mwa mengine na zaidi ya yote, kuboresha maisha ya Waafrika wa kawaida," Muchanga amesema.
Muchanga amesisitiza haja ya kujenga taasisi na kutekeleza sera sahihi zinazoweka mazingira wezeshi ya biashara kwa ajili ya urasimishaji wa sekta binafsi pamoja na kuimarisha uwiano wa sera ya viwanda unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji bora wa programu na miradi ya maendeleo ya viwanda kupitia ufuatiliaji na tathmini ipasavyo ya matokeo.
Amesema, kwa kuzingatia mahitaji hayo, AU inapendekeza kuteuliwa kwa Mhamasishaji wa AU katika Uanzishaji wa Viwanda na Mabadiliko yenye tija, ambaye atatoa uongozi wa kisiasa, kuongeza uelewa na kuhakikisha utekelezaji mzuri wa maendeleo ya viwanda barani Afrika.
Aidha amebainisha kuwa miundombinu na nishati ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda, huku akiangazia hali mbaya ya umeme, maji, barabara na teknolojia ya habari na mawasiliano barani Afrika.
Amebainisha kuwa upungufu wa miundombinu "unaweka gharama kubwa kwa viwanda kwa kupunguza ushindani, ambao unazuia upatikanaji wa masoko ya ndani na ya kimataifa."
"Afrika inakabiliwa na pengo kubwa la miundombinu, ambapo ni asilimia 4 tu ya Pato la Taifa la Bara linalotengwa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu kila mwaka," Muchanga amesema.
Kamishna huyo wa AU amesisitiza maendeleo ya miundombinu kama jambo muhimu katika kupata maendeleo.
“Ni wazi kuwa kuziba pengo la miundombinu ni muhimu katika kufungua uwezo wa kiviwanda barani Afrika, ambao ukitumiwa, unaweza kuongeza ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 2 kila mwaka,” amesema.
Pia ameangazia haja ya kuwa na mbinu mwafaka za ufadhili na uwekezaji kusaidia ukuaji wa viwanda barani Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma