

Lugha Nyingine
China yalaani hatua ya Marekani kushinikiza nchi nyingine kujiunga na vikwazo vya teknolojia
BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian siku ya Jumatatu amekosoa mpango wa Marekani wa kuishinikiza Japan na Uholanzi kujiunga nayo ili kuzuia mtiririko wa teknolojia ya hali ya juu ya chipu kwenda China.
"Hii siyo tabia ambayo nchi kubwa iliyo wazi na ya uaminifu inaweza kuonesha," Zhao ameuambia mkutano na wanahabari alipoulizwa kutoa maoni yake juu ya hatua hiyo ya Marekani.
Lakini tena, hakuna jambo jipya kuhusu jinsi Marekani inavyotumia vibaya mamlaka yake ya serikali na faida ya kiteknolojia na kuwalazimisha washirika wake kiuchumi ili tu kuendeleza umwamba wake wa kivita na maslahi binafsi, amesema.
Zhao amesema Marekani inaendelea kuingiza siasa katika masuala ya teknolojia na biashara, na kuyageuza kuwa silaha na kuyaweka kwenye itikadi.
"Dunia inaona kwa uwazi kile Marekani inachofanya. Yeyote anayejaribu kuzuia njia ya wengine atakuwa amezuiliwa njia yake mwenyewe," amesema.
Ametoa wito kwa pande husika kuchukua msimamo wenye ukweli na haki, kuzingatia maslahi yao ya muda mrefu na maslahi ya kimsingi ya jumuiya ya kimataifa na kufikia hitimisho sahihi, kwa uhuru bila shinikizo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma