China yaongeza juhudi za kukabiliana na ukame ili kuhakikisha uzalishaji, shughuli za watu kujipatia kipato
NANCHANG - Mabomba yenye urefu wa kilomita tatu kwenye milima, yakibeba maji hadi kwenye kijiji cha milimani cha Dougang. Nie Xiaolong, akiwa amesimama karibu na mwisho wa bomba na mikono yake ikiwa imeshika kiuno chake anajisikia faraja kuona maji yakielekezwa kwenye mashamba yake.
Muda mfupi uliopita, Nie mwenye umri wa miaka 42, alikuwa na wasiwasi kuhusu hekta 200 za mazao anazosimamia katika eneo la Mji wa Ruichang, Mkoa wa Jiangxi, nchini China kutokana na ukame uliosababishwa na hali ya hewa ya joto na mvua kidogo iliyodumu kwa wiki kadhaa.
"Nilidhani labda nisingeweza kufanikiwa," Nie anasema. "Shukrani kwa serikali ya mtaa kwa msaada wa kufunga pampu za maji na kutandaza mtandao wa mabomba, mazao yangu yameokolewa."
Mawimbi ya joto yameenea katika sehemu nyingi za China msimu huu wa joto. Jumatatu, ikiwa ni siku ya 11 mfululizo, Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa ya China imeendelea kutoa tahadhari nyekundu kwa joto la juu, ambayo ni tahadhari kali zaidi katika mfumo wa tahadhari za hali ya hewa wenye ngazi nne wa China.
Huku zikikabiliwa na uhaba wa maji na ugavi wa umeme katika mikoa iliyoathiriwa na ukame, serikali za ngazi zote nchini China zimeongeza juhudi za kukabiliana na ukame na kuhakikisha uzalishaji wa kawaida na shudhuli za watu za kujipatia kipato.
Kuhakikisha umwagiliaji kwenye shughuli za kilimo
Mkoa wa Jiangxi ni nyumbani kwa Ziwa Poyang, ziwa kubwa zaidi la maji safi ya China. Mnamo Agosti 6, ziwa hilo liliingia rasmi katika msimu wa kiangazi wa mwaka huu, ikiwa ni tarehe ya mapema zaidi tangu utunzaji wa rekodi uanze Mwaka 1951 na siku 69 mapema kuliko wastani wa tarehe ya kuanza kati ya Mwaka 2003 na 2021.
Picha iliyopigwa Agosti 17, 2022 kutoka angani ikionyesha kisiwa kidogo cha Luoxingdun kikichomoza kwenye ulalo wa Ziwa la Poyang uliokauka katika Mkoa wa Jiangxi nchini China. (Xinhua/Wan Xiang)
Kwa mujibu wa Idara ya Rasilimali ya Maji ya Mkoa wa Jiangxi, kufikia saa 8 asubuhi Jumatatu, eneo la maji la ziwa hilo lilikuwa na jumla ya kilomita za mraba 575, ikiwa ni kilomita za mraba 2,475 chini ya zile za miaka iliyopita,.
Hata hivyo, katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Jiangxi, zaidi ya vituo 15,000 vya kusukuma maji na zaidi ya seti 308,000 za vifaa vya kuhamishika vya kukabiliana na ukame vimewekwa tayari, pamoja na juhudi nyingine, ambazo zimepunguza upotevu wa nafaka zenye thamani ya karibu yuan bilioni 3 (kama dola milioni 440 za Marekani).
Wizara ya Kilimo na Vijiji imetuma vikundi kazi na timu za kisayansi na kiteknolojia kwa mikoa muhimu kwa uzalishaji wa nafaka na iliyoathiriwa na wimbi la joto ili kutoa mwongozo kuhusu misaada ya ukame.
Wakulima wakimwagilia mimea ya mazao katika Kijiji cha Beiping, Eneo la Cili, Mkoa wa Hunan, nchini China, Agosti 17, 2022. (Xinhua/Zhang Ge)
Wizara ya Rasilimali za Maji ilitangaza wiki iliyopita kwamba mabwawa katika maeneo ya juu na ya kati ya Mto Changjiang , hasa Bwawa la Mabonde Matatu katikati mwa Mkoa wa Hubei nchini China, yatarejesha zaidi mita za ujazo bilioni 1.48 za maji katika maeneo ya chini, kuanzia Agosti 16. Hapo awali, mita za ujazo bilioni 5.3 za maji zilikuwa tayari zimetolewa mwezi Agosti.
Kukidhi mahitaji ya maji na nishati ya umeme
"Lori la kunyunyizia maji linakuja! Tafadhali ingia kwenye foleni," wafanyakazi wa kijamii waliwaambia watu wengi waliokuwa wakisubiri lori hilo likiingia katika Kijiji cha Guangdong cha Eneo la Cili, Mkoa wa Hunan nchini China.
Wu Yanglin, pamoja na baadhi ya wanakijiji, walisimama kando ya barabara wakiwa na ndoo za maji mkononi. "Shinikizo la maji ni dogo katika nyumba yangu kwani hifadhi ya maji kijijini sasa ina hifadhi ndogo ya maji. Tumekuwa tukiishi bila maji ya bomba kwa siku nyingi," anasema Wu.
Picha iliyopigwa Agosti 16, 2022 kutoka angani ikionyesha askari wa zimamoto wakipeleka maji kwa wanavijiji katika Eneo la Makazi la Zhenzhu huko Wuchuan, Mkoa wa Guizhou nchini China. (Picha na Luo Xinghan/Xinhua)
Kando na msaada uliotolewa na mradi wa kujaza maji kwenye Mto Changjiang, kiasi cha yuan milioni 210, ambazo ni fedha za kusaidia maafa zimetengwa na Wizara ya Fedha na Wizara ya Usimamizi wa Dharura kwa ajili ya maeneo saba ya ngazi ya mkoa ili kudhibiti ukame, kwa kuzingatia kutatua uhaba wa maji majumbani.
Ukiwa ni mzalishaji mkuu wa nishati ya maji nchini China, Mkoa wa Sichuan, Kusini-Magharibi mwa China umekumbwa na joto jingi tangu Mwezi Julai na kushuhudia wastani wa kunyesha kwa kuvua ukifikia asilimia 51 chini ya ule wa kipindi kama hicho miaka ya nyuma.
Mkoa unafanya kila juhudi kuhakikisha kila familia ina umeme, na kuhimiza wafanyabiashara kuepuka kutumia umeme wakati wa matumizi makubwa. Wafanyakazi 25,000 wa ukarabati wa dharura wa umeme wamekuwa wakisubiri saa 24 kwa siku.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma