Tanzania yasisitiza dhamira ya kuhifadhi bahari na rasilimali za baharini
DAR ES SALAAM - Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, Jumatatu wiki hii amesisitiza dhamira ya serikali ya nchi hiyo ya uhifadhi endelevu na matumizi ya bahari na rasilimali za majini.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania imesema Mpango ametoa ahadi hiyo alipohutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari huko Lisbon, Ureno.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mpango amesema mbali na kuridhia mikataba ya kimataifa ya kudhibiti uchafuzi wa baharini, Tanzania imeandaa sera, mikakati na mipango ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Amesema Tanzania pia imechukua hatua, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kabisa matumizi ya mara moja ya mifuko ya plastiki ambayo ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa baharini kote duniani.
“Pia tumetunga sheria zinazoongoza usimamizi wa rasilimali za pwani na baharini,” amesema na kuongeza kuwa Tanzania pia imetekeleza miradi inayohusu kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kurejesha mifumo ya ikolojia ya pwani na baharini.
Mpango ametaja hatua nyingine za uhifadhi kuwa ni kudhibiti uvuvi wa kutumia milipuko kwa karibu asilimia 99 na kuimarisha udhibiti na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi kwenye bahari kuu.
Eneo la maji la Tanzania lina ukubwa wa kilometa za mraba 64,000, hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa tajiri kwa bayoanuwai yenye uwezo mkubwa wa uchumi wa bluu ambao unasaidia maisha ya mamilioni ya watu wake, ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula na usafiri.
Hata hivyo, Mpango amesema, kufaidika ipasavyo kiuchumi na sekta hii ya bahari kunaathiriwa na uchafuzi wa mazingira ya bahari, upotevu wa viumbe hai na makazi ya majini, athari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi na mmomonyoko wa fukwe.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma