

Lugha Nyingine
Kenya yatangaza kifo cha simba dume maarufu Sirikoi
NAIROBI – Shirika la Huduma ya Wanyamapori la Kenya (KWS) Jumamosi lilitangaza kifo cha simba dume mwenye haiba kwenye makazi yake ya asili ndani ya Mbuga ya Taifa ya Nairobi kutokana na ugonjwa ambao haukutajwa.
Taarifa ya KWS iliyotolewa mjini Nairobi, Mji Mkuu wa Kenya inasema kuwa simba huyo mkubwa aitwaye Sirikoi alizaliwa Januari 2014 katika Bonde la Sosia, lililoko Kaskazini-Magharibi mwa Kenya kaunti ya Laikipia. Alitoka kwenye familia ya MF, ambayo ni ya simba wenye mvuto na nguvu.
Kwa mujibu wa KWS, Sirikoi alikuwa simba mkubwa mwenye mbinu na ujuzi mkubwa wa kuwinda ambao ulimwezesha kushambulia na kuua mawindo wakubwa kama vile twiga na nyati akiwa peke yake.
"Hasa, alikuwa na manyoya meusi ambayo ni kiashirio kikubwa cha afya ya simba, ari na nguvu pamoja na viwango vya testosterone," imesema KWS.
Kabla ya kifo chake, Sirikoi alikuwa amezaa watoto pamoja na Simba wenzake wa kike katika Mbuga ya Taifa ya Nairobi, hifadhi ya wanyamapori iliyoko kwenye ukingo wa Kusini-Mashariki mwa Nairobi.
Taarifa ya KWS inasema, simba huyo mashuhuri atatiwa mumiani, ili kukaushwa na kuhifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Taifa la Kenya.
Kwa mujibu wa sensa ya wanyamapori iliyofanywa na Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Kenya na kutolewa Agosti 2021, idadi ya simba nchini humo ilifikia 2,000 lakini wanyama hao wanaokula nyama walikuwa wakikabiliana na vitisho vingi ikiwa ni pamoja na upotevu wa makazi, ujangili, na magonjwa na mishtuko inayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma