

Lugha Nyingine
Afisa wa Umoja wa Mataifa asema mgogoro kati ya Ukraine na Russia unaathiri ufanisi wa uchumi wa Afrika
NAIROBI - Mwakilishi mkazi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Kenya, Walid Badawi amesema jana Jumanne kwamba mgogoro kati ya Ukraine na Russia unaathiri vibaya ufanisi wa uchumi wa Afrika.
Badawi amesema kuwa mgogoro huo umesababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa za msingi katika bara hilo.
"Nchi nyingi barani Afrika ni waagizaji wa jumla wa chakula na wanategemea sana mauzo ya ngano kutoka Russia na Ukraine. Mnyororo huu wa thamani sasa umeathiriwa na unaweza kusababisha kuongezeka kwa ukosefu wa usalama wa chakula," Badawi amesema mjini Nairobi, Mji Mkuu wa Kenya, pembezoni mwa kongamano la ngazi ya juu kuhusu uhamasishaji wa uwekezaji katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) kwa Afrika.
Amesema tangu mgogoro kati ya Ukraine na Russia ulipozuka mwezi Februari, gharama za nishati ya mafuta katika masoko ya kimataifa zimeongezeka na hii imesababisha gharama za nishati katika bara hilo kuwa kubwa.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa mgogoro huo umesababisha kuchepushwa kwa misaada ya maendeleo kutoka Afrika kwenda kwa nchi zilizoathiriwa na mgogoro huo.
"Nchi nyingi za Ulaya zimeathiriwa moja kwa moja na wimbi la wakimbizi kutoka Ukraine na sasa zinaelekeza upya bajeti zao za misaada ya maendeleo ya ng'ambo ili kushughulikia shinikizo zao za ndani kwa sababu zinapaswa kuwahudumia wakimbizi," Badawi ameongeza.
Ameeleza kuwa nchi zenye uchumi mkubwa na wahisani wa kutegemewa pia wametangaza kupunguza bajeti ya Umoja wa Mataifa.
"Hii itakuwa na madhara makubwa katika uwezo wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ya maendeleo katika kufadhili juhudi za kupunguza umaskini barani Afrika," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma