Mji Mkuu wa China, Beijing waongeza vizuizi ili kukabiliana na maambukizi mapya ya UVIKO-19
Mhudumu wa Afya akichukua sampuli kutoka kwa mkaazi kwa ajili ya kupima virusi vya Korona katika eneo la Daxing, Beijing, Mji Mkuu wa China, Aprili 30, 2022. (Xinhua/Peng Ziyang)
BEIJING - Mji Mkuu wa China, Beijing jana Jumamosi umetangaza kuongeza hatua mpya za vizuizi dhidi ya UVIKO-19 ili kupunguza maambukizi ya virusi hivyo, kwani safari nyingi za watu zinatarajiwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakati wa likizo ya siku tano ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyoanza rasmi jana Aprili 30.
Beijing imeripoti maambukizi mapya yaliyothibitishwa ya virusi vya Korona yapatayo 59 na visa vinane vya wagonjwa wa UVIKO-19 wasioonesha dalili za kuumwa kati ya Saa 9 alasiri siku ya Ijumaa na 9 alasiri Jumamosi. Jumla ya maambukizi 295 katika maeneo 13 yameripotiwa katika mji huo tangu Aprili 22.
Beijing sasa ina maeneo sita yaliyotangazwa kuwa yenye hatari kubwa na maeneo 23 yenye hatari ya wastani ya UVIKO-19.
Kwa mujibu wa Ding Jianhua kutoka Idara ya Biashara ya Mji wa Beijing, maambukizi mengi ya UVIKO-19 katika wimbi jipya la hivi karibuni yametokea kwenye mikahawa. Kwa hivyo, ili kupunguza hatari ya maambukizi, mikahawa yote katika Mji wa Beijing itasitisha kuhudumia chakula ndani ya mikahawa na badala yake itatoa huduma kwa kuagiza oda kwa watu nyumbani kuanzia Mei 1 hadi 4.
Beijing pia inajiandaa kujenga hospitali za muda kwa ikiwa zinahitajika.
“Hadi kufikia sasa, takriban vitanda 4,000 vimeandaliwa maalumukwa wagonjwa wa UVIKO-19, na maeneo zaidi yamebadilishwa kuwa hospitali kubwa za muda ikiwa italazimu” Li Ang, Naibu Mkurugenzi wa Kamati ya Afya ya Mji wa Beijing, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Jumamosi.
"Hospitali za muda zimejengwa kwa ajili ya kutibu wagonjwa wenye dalili kidogo na wale wasio na dalili za ugonjwa, ambayo ni njia madhubuti ya kuzuia kuenea kwa janga hili. Pia ni muhimu kupunguza matumizi mabaya ya rasilimali za matibabu na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu kwa wakati," Li amesema.
Li ameongeza kuwa wakazi hawapaswi kuogopa kwani kwa sasa "hakuna wagonjwa wengi sana hapa Beijing, lakini tunapaswa kupanga mapema."
Matokeo hasi ya vipimo vya virusi vya Korona yanahitajika ili kuruhusiwa kuingia katika maeneo ya umma wakati wa likizo ya Siku ya Wafanyakazi.
Bustani, maeneo ya wazi ya burudani na shughuli za kitamaduni zinatakiwa kuweka vikomo vya idadi ya wageni kwa nusu ya uwezo wa juu wakati wa likizo hiyo.
Serikali ya Mji wa Beijing pia inawataka watu wanaoingia katika maeneo ya umma au kuchukua usafiri wa umma kufanya vipimo vya Virusi na kuthibitisha hawana maambukizi ndani ya siku saba kuanzia Mei 5. Upimaji wa virusi hivyo utatolewa kwa wananchi bila malipo kuanzia Mei 3 ili kurahisisha umma kutekeleza zoezi hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma