Katibu Mkuu wa UN apendekeza njia 5 za kufufuka kwa Uchumi na maendeleo ya nchi zenye maendeleo duni
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Mkutano wa tano wa Nchi Zenye Maendeleo Duni (LDCs) kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Machi 17, 2022. (Loey Felipe/Picha/Kitini cha Umoja wa Mataifa kupitia Xinhua)
UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Alhamisi wiki hii amependekeza njia tano ambazo zitasaidia uchumi wa nchi zenye maendeleo duni (LDCs) kufufuka katika muda mfupi, kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu katika muda wa kati, na kustawi kwa muda mrefu.
“Njia ya kwanza ya ni usambazaji ulio sawa wa chanjo dhidi ya UVIKO-19” amesema.
Ameitaja njia ya pili kuwa ni mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao unaweka kipaumbele kwenye mahitaji ya nchi zenye maendeleo duni.
Amesema kwamba, nchi zinazoendelea zinahitaji kuwekeza zaidi katika sekta muhimu kuliko hapo awali ili kupunguza umaskini na kuongeza uimara katika uchumi. Lakini hizi sekta muhimu haziungwi mkono na mfumo mbovu wa kifedha wa kimataifa ambao unakwamisha jitihada hizo.
Amesema, nchi hizo zinahitaji kusamehewa madeni, kupitia upya mikataba yao ya madeni na kufutiwa madeni. Zinapaswa kuweza kukopa kwa riba ya chini na kulindwa wakati wa majanga, ikiwa ni pamoja na kuweka vifungu vinavyohusu vimbunga katika mikataba ya madeni. Pia kuna haja ya kuongeza ukwasi unaopatikana kwa LDCs na kuunda mfumo wa haki wa ushuru na kupambana na fedha haramu.
Guterres amesema, njia ya tatu ni kusaidia mabadiliko ya muundo wa uchumi katika LDCs.
Amesema kwamba, ukuaji wa uchumi katika nchi hizi unahusishwa kwa kiwango kikubwa na maliasili au sekta za uchimbaji madini, ambazo ni tete sana kwa muda mfupi na zinaweza kuathiriwa na kubadilika kwa bei ya bidhaa, matakwa ya soko, na mabadiliko ya tabianchi.
“LDCs zinahitaji kusaidiwa kubadilisha miundo na mifumo ya kiuchumi. Zinahitaji kuungwa mkono ili kuongeza ushiriki wao katika minyororo ya thamani ya kimataifa. Hii ina maana kuwekeza kwa wafanyakazi wenye afya, elimu na ujuzi. Inamaanisha kuboresha miundombinu na mitandao ya usafirishaji na kuwezesha mtiririko wa biashara ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi. Inamaanisha kutambua manufaa ya muunganisho wa kidijitali kwa wote ili biashara ziweze kushindana na kustawi katika uchumi wa Dunia. Inamaanisha kubadilisha sekta za uchimbaji madini na kuunda nafasi za kazi za kijani na uchumi wa kijani. Na ina maana ya kukuza sheria za biashara iliyo wazi na ya haki ili nchi zote ziweze kushindana katika uwanja sawa, bila kujali nafasi zao katika ngazi ya maendeleo” amesema.
Ameitaja njia ya nne ya kuboresha hali ya maisha kuwa ni hatua za mabadiliko ya tabianchi. “Nchi zenye maendeleo duni hazikusababisha athari za tabianchi. Lakini zinaishi na athari zake mbaya zaidi” amesema.
Njia ya tano ni amani na usalama. Guterres amesema, Dunia kwa sasa inakabiliwa na idadi kubwa zaidi ya migogoro mikali tangu Mwaka 1945. Na LDCs zinachukua sehemu kubwa ya maeneo haya yenye migogoro ya kivita.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kwenye jukwaa na kwenye skrini) akihutubia Mkutano wa tano wa Nchi Zenye Maendeleo Duni (LDCs) kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mnamo Machi 17, 2022. (Loey Felipe/Picha/Kitini cha Umoja wa Mataifa kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma